Serikali ya kaunti ya Kisii imeanzisha mradi wa kupanda miti 10,000 ili kuimarisha mazingira ya kaunti hiyo.
Akizungumza mnamo siku ya Jumatatu mjini Kisii waziri wa mazingira katika kaunti hiyo Omoiro Omari alisema serikali hiyo iliamua kupanda miti 10,000 ili kuimarisha mazingira na hewa safi ambayo ni nzuri kwa maisha ya binadamu.
Upanzi wa miti hiyo utafanywa katika ofisi za serikali ya kaunti hiyo, shule zote pamoja na mahospitali.
Waziri huyo alisema kuwa hiyo ndio njia mojawapo ya kudumisha mazingira mema katika kaunti ya Kisii ambayo ni ya kupendeza kwa hewa safi.
“Tutapanda miti katika mashule, mahospitali na katika ofisi za uma ili kuimarisha mazingira mema na tayari upanzi huo umeanza,” alisema Omari.
Hata hivyo waziri Omoiro alitangaza kuwa mnradi huo utawasadia idadi nyingi ya vijana ili kujiendeleza, kwani idadi nyingi itaenda kujinufaisha kwa kukabidhiwa kibarua hicho ii kupata riziki ya kila siku.
“Mradi huu wa kupanda miti utawasaidia vijana wengi watakaosaidia serikali kupanda miti ili waweze kupata riziki ya kila siku na kujiendeleza,” aliongezea Omoiro.
Sasa serikali ya kaunti hiyo, imetangaza kudumisha usafi na mazingira mema ambayo ni ya manufaa kwa maisha ya binadamu kupitia upanzi wa miti hiyo.