Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wa Kaunti ya Mombasa wameilaumu serikali ya kaunti hiyo kwa kushindwa kulitatua tatizo la uhaba wa maji linaloingia wiki ya pili sasa.

Wakazi hao, wakiongozwa na Salim Nyoka, wamesema kuwa hatua hiyo imechangiwa na uongozi duni kutoka kwa serikali hiyo licha ya wakazi hao kulipa ada za maji kila mwezi.

Wakizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, wakazi hao wamesema kuwa wanapitia hali ngumu kupata maji safi, na wanahofia kuwa huenda wanaouza maji kwa kutumia mkokoteni wakawauzia wakazi maji taka na kusababisha maradhi ya kiafya.

"Sisi tunashangazwa na serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa kushindwa kulitatua tatizo la uhaba wa maji Mombasa kwa zaidi ya wiki mbili sasa, na sisi wakazi wa Mombasa tunalipa ada za maji kila mwezi, sasa tunaitaka serikali ya kaunti kupitia waziri wa mazingira na raslimali za maji kuchukua hatua za haraka na kusuluhisha tatizo hilo," alisema Nyoka.

Hata hivyo, wamesisitiza kwamba Kaunti ya Mombasa inakabiliwa na hali ngumu ya kifedha kwani bodi ya usambazaji maji eneo la Pwani inaidai kaunti hiyo shilingi milioni 600.