Share news tips with us here at Hivisasa

Kaunti ya Uasin-Guishu tayari imeanza kutumia kima cha shilingi milioni 200 ambazo zilitengwa kukabiliana na athari za mvua ya El~Nino.

Licha ya kuwa athari za mvua hiyo bado hazijaanza kuonekana, tayari utawala huo umeanza kutumia fedha hizo hasa kwa kuajiri vijana kufungua na kupanua mitaro ya kupitisha maji taka.

Kwa mujibu wa waziri wa mazingira, maji na kawi katika kaunti hiyo Mary Njogu akizungumza Jumanne, mradi huo ni mojawapo ya mikakati ya kaunti kukabiliana na athari za mvua hiyo.

“Kutumia fedha hizi katika kusafisha mitaro ya maji taka si hatia, kwani kazi hii ni sehemu ya mipango ya kaunti ya kukabiliana na athari za mvua hii ambayo imeanza kunyesha katika kaunti hii” alisema Njogu

Njogu alisema fedha hizo hazitatosheleza mikakati ya kaunti hiyo kukabiliana na El~Nino ndiposa wametaka serikali kuu kuiongezea kaunti hiyo Sh200 milioni zaidi kukabiliana na aathari za mvua hiyo.

Alisema tayari utawala huo umeorodhesha maeneo yote ambayo yanatishiwa na athari za mvua hiyo msimu huu.

Viongozi kutoka kaunti hiyo wamewataka watu ambao wanaishi katika maeneo ambayo yanatishiwa na mafuriko kuhama mapema ili kuzuia kutokea kwa maafa wakati mvua hiyo itakaposhika kasi.