Serikali ya kaunti ya Kisii imepokezwa soko sita za kisasa ili kuwa chini ya usimamizi wake baada ya kujengwa na serikali ya kitaifa.
Soko hizo ambazo zilijengwa kwa njia ya kisasa zitakuwa chini ya uongozi wa serikali ya kaunti ya Kisii, ambayo itachukua usimamizi pamoja na shughuli zote za kibiashara.
Soko hizo zilikabidhiwa serikali ya kaunti hiyo siku ya Jumanne katika eneo la Riosiri kupitia waziri wa kilimo na ufugaji nchini Willy Bett .
Miongoni mwa soko hizo ni soko la Rioma, ambalo liko eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini, soko la Mosocho liliko eneo bunge la kitutu Chache kusini, soko la Kiamokama eneo bunge la Nyaribari Masaba, soko la Kenyenya eneo bunge la Bomachoge chache, soko la Riosiri, katika eneo bunge la Mugirango kusini na soko la Riombongi.
Wakati huo huo, gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae alipongeza serikali ya kitaifa kwa juhudi hizo za kuhakikisha soko za kisasa zimejengwa katika kaunti hiyo kupitia serikali ya kitaifa ili kuimarisha mazingira ya wafanyibiashara.
“Napongeza serikali kuu kwa kazi nzuri ambayo imefanya ya kuhakikisha wafanyibiashara wetu wanafanya huduma zao za kibiashara kwa mazingira bora,” alisema Ongwae.