Kaunti ya Uasin Gishu imekusanya zaidi ya shilingi millioni 800 kutokana na ushuru wa mapato kwa kipindi kisichopungua miezi kumi.
Gavana wa Kaunti Bw Jackson Mandago alisema licha ya ufanisi huo, kaunti hiyo ililenga kukusanya zaidi ya shilingi billioni moja kwa kipindi hicho.
“Wakati tulipoingia afisini, iliokuwa manispaa ya Eldoret ilikuwa ikikusanya shilingi millioni 600 kwa mwaka kama ushuru wa mapato, lakini tulipoingia kama utawala wa kaunti, tulikusanya shilingi takribani millioni 800," alisema Mandago.
Akihutubia wanahabari ofisini mwake siku ya Jumanne, Gavana Mandago alielezea matumaini ya kukusanya zaidi ya shilingi billioni moja katika kipindi cha bajeti ya mwaka huu wa 2015/2016.
Bw Mandago alisema ufanisi huo unatokana na juhudi za utawala wake kunoa makali dhidi ya ufisadi katika sekta ya ukusanyaji ushuru.
Kiongozi huyo alisema sehemu kubwa ya ushuru huo ilitokana kwa wafanyibiashara katika sekta mbali ikiwa ni pamoja na sekta ya magari ya uchukuzi wa abiria.
Hata hivyo, Bw Mandago alionya maafisa wa ukusanyaji ushuru katika kaunti hiyo dhidi ya kuingiza ufisadi katika kaunti hiyo.
Miaka miwili iliopita kaunti hiyo ilisimamisha kazi maafisa wa ukusanyaji ushuru ambao walinaswa wakiwa wameficha pesa kutoka kwa wafanyibiashara.