Serikali ya kaunti ya Nyamira imelaumiwa kwa kusimamisha shughuli ya kupima ugonjwa wa saratani katika kaunti hiyo jinsi ilivyopangwa hapo awali.
Hii ni baada ya idadi kubwa ya wakazi kujitokeza kupimwa ugonjwa wa saratani katika hospitali ya Level Five mjini Nyamira siku ya Alhamisi na kupata shughuli hiyo imesimamishwa kwa sababu zisizojulikana.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika hospitali hiyo ya Nyamira, wakazi hao walilaumu serikali ya kaunti kwa kutoweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kile walichokipanga awali kimefanywa kikamilifu.
Aidha, walisema wengi wao walitumia nauli kutoka makwao wakiwa na nia ya kupimwa ugonjwa wa saratani ili kujua hali zao.
“Serikali ya kaunti imetukosea sana maana ilitangaza kuwa siku ya leo, Alhamisi, shughuli ya kupima ugonjwa wa saratani ingefanyika hapa Nyamira, na tumefika tukapata hakuna chochote kinaendelea,” alisema Joshua Nyakoe, mkazi.
Shughuli hiyo ya kupima ugonjwa wa saratani ingefanyika kati ya ushirikiano wa serikali ya kaunti hiyo na shirika la Health Care Rescue Centre.
“Sisi tunajua serikali yetu kila wakati inashindwa kutimiza ahadi, uchungunzi wetu ambao tumefanya tangu tufike hapa kwa hospitali ni kuwa serikali haikuwa na pesa za kugharamia wageni ambao wangefanya hii shughuli kutoka Nairobi na penye watalala, tunaomba serikali hii iwe inajipanga kikamilifu," alisema Bethuel Osankia, mkazi mwingine.