Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kaunti ya Kisii imeombwa kujenga chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Marani iliyoko eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini ili kurahisishia wakaazi wa eneo hilo kibarua cha kutembea hadi mjini Kisii kuhifadhi wapendwa wao wanapofariki.

Wakizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumapili mjini Marani idadi nyingi ya wakaazi wakiongozwa na Dickson Onsarigo waliomba serikali ya kaunti ya Kisii kuwapunguzia mzigo wa gharama wanapohifadhi wapendwa wao katika hospitali ya rufaa ya Kisii na zingine ambazo ziko mjini Kisii kwa kuwajengea chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Marani.

Hata hivyo, walisema wamekuwa wakigharamika kwa muda mrefu wanapowasafirisha wapendwa wao nyumbani kutoka hifadhi ya hospitali zilioko mjini Kisii kwani hutumia pesa nyingi na kuomba kupunguziwa mzigo huo.

“Tunaomba serikali yetu ya kaunti kutusaidia kujenga chumba cha kuifadhi maiti katika hospitali yetu ya Marani kwani hospitali hii imekuwa hapa kwa muda mrefu bila kuwa na chumba hicho,” alisema Onsarigo.

“Huwa tunagharamika sana tunapoenda kupata huduma hiyo katika hospitali ya rufaa ya Kisii kwani ni mbali na kwetu, ” aliongeza Onsarigo.

Wakati uo huo, wakaazi hao waliomba serikali ya kaunti kuleta dawa za kutosha katika hospitali hiyo kwa kile walichokisema wanapoenda kuhudumiwa kimatibabu hulazimika kutumwa kwa zahanati zilizoko karibu kununua dawa, jambo ambalo halipendezi kwao na kutaka kusaidiwa na serikali ya kaunti kwani sekta ya afya iko chini ya usimamizi wa kaunti.

Jukumu ni la serikali ya kaunti kuwasaidia wakaazi hao kwa kuitikia wito huo na kufanya jinsi wanavyohitaji ili kutoa msaada.