Serikali ya Kaunti ya Kisii imeombwa kuharakisha na kukamilisha miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa kabla ya kuanzisha miradi mingine mipya ya maendeleo katika wadi mbalimbali za kaunti hiyo.
Hii ni baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo imeonekana kukwama huku miradi mingine mipya ikibisha.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Kisii, mwakilishi wa wadi ya Magenche, eneo bunge la Bomachoge Borabu Timothy Nyarang’o alisema ikiwa serikali ya kaunti hiyo inahitaji kufaulu katika miradi ya maendeleo, sharti ikamilishe kila mradi kwa wadi zote kabla ya kuanzisha miradi mingine mipya.
“Naomba serikali ya Kaunti ya Kisii kukamilisha miradi yote iliyoanzisha kwa wadi zetu kabla ya kuanzisha miradi mingine mipya ya maendeleo ili kuleta usawa katika maendeleo,” alisema Nyarang’o.
“Naomba miradi hiyo kuharakishwa ili kaunti yetu iweze kufanya maendeleo mengi zaidi kabla ya uchaguzi ujao wa mwaka 2017,” aliongeza Nyarang’o.
Wakati huo huo, Nyarang’o alisema kuna baadhi ya barabara ambazo hazijakamilika kukarabatiwa katika wadi yake na kuomba serikali ya kaunti hiyo kuharakisha kuifanya sawia na wadi zingine.
Jukumu ni la serikali ya kaunti hiyo kuitikia wito huo wa kuharakisha na kukamilisha m iradi hiyo ya maendeleo kabla ya miradi mingine.