Waendeshaji bodaboda mjini Nyamira wameiomba serikali ya Kaunti ya Nyamira kujali maslahi yao na kukarabati barabara ambazo ni mbovu zaidi katika kaunti hiyo.
Kulingana na wanabodaboda hao, barabara nyingi hazipitiki mvua inaponyesha, na kuwapelekea kusimamisha biashara zao za uchukuzi.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano mjini Nyamira, waendeshaji hao wakiongozwa na mwenyekiti wao Wycliffe Ongaga walisema barabara nyingi ni mbovu, na kuomba serikali ya kaunti kuwakarabatia barabara ambazo zimeharibika ili kuendelea kufanya biashara zao bila tashwishi.
“Barabara nyingi za kaunti hii hazipitiki mvua inaponyesha, tunaomba serikali ya kaunti kutukarabatia ili sekta yetu ya uchukuzi iimarike zaidi,” alisema Ongaga.
Miongoni mwa barabara ambazo walidai kuwa mbaya ni Manga-Riamogambi, Kahawa-Kineni na zingine ambazo waliomba kukarabatiwa.
Wakati huo huo waendeshaji bodaboda hao walikosoa serikali ya kaunti hiyo kwa kuwapa ahadi za uongo kwani walidai kuwa serikali ya kaunti iliwahidi kuwajengea vibanda mbalimbali mjini Nyamira ili wawe wanajikinga mvua inaponyesha.
“Tunaomba serikali itimize ahadi ilizotoa maana tunasumbuka mvua inaponyesha, hatuna mahali pa kupumzikia wakati wateja hawako tunaomba vibanda vile tuliahidiwa tujengewe ikiwa serikai inajali maslahi ya wanabodaboda,” alisema Erick Mokworo mwanabodaboda mwingine.