Serikali ya kaunti ya Nyamira imeombwa kusimamisha ujenzi wa soko la Mosobeti lililoko katika kaunti hiyo.
Hii ni baada ya soko hilo kusemekana kutokuwa na msingi unaofaa jambo ambalo limezua maswali baina ya wanakamati wa soko hilo na wafanyibiashara wengine.
Wakizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumatano katika soko hilo, wanakamati wa soko hilo la Mosobeti wakiongozwa na naibu mwenyekiti wa wanakamati hao Elijah Okong’o na Tom Omweri walisema jinsi ujenzi wa soko hilo umeanzishwa hauna msingi unaofaa huku wakisema huenda jengo la soko hilo likaanguka kabla ya miezi mitano kukamilika na kuomba serikali ya kaunti ya Nyamira kuingilia kati na kusimamisha ujensi huo ili kuanzishwa upya.
“Hakuna msingi unaofaa katika ujenzi wa soko hili la Mosobeti , jinsi ujenzi umeanzishwa katika soko hili si halali tumeofya sana na tunaomba serikali kuingilia kati kusimamisha ujenzi huu ili kuanzishwa upya,” alisema Elijah Okong’o, naibu mwenyekiti wa kamati inayosimamia soko hilo.