Watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti ya Nakuru wamepata afueni kubwa baada ya serikali ya kaunti hiyo kuzindua hazina itakayowapa fedha za kujiendeleza kiuchumi.
Hazina hiyo, ‘Nakuru County Persons With Disability Fund’, imewezesha kutengwa kwa shilingi milioni 55, ambazo zitatumika katika wadi zote za kaunti hiyo kuboresha maisha ya kikundi hicho.
Akiongea mjini Nakuru Jumatano, mwakilishi wa walemavu katika bunge la kaunti ya Nakuru Emma Mbugua, alisema kaunti hiyo ina wadi 55, kumaanisha kila wadi itapata shilingi milioni moja.
Kulingana na kiongozi huyo, mikakati ambayo inawekwa sasa kabla ya fedha hizo kuachiliwa rasmi ni kuundwa kwa kamati ya walemavu katika kaunti nzima, na kisha kamati zingine kama hiyo katika kila wadi.
Kazi ya kamati hizo itakuwa ni kuhakikisha usajili wa walemavu unafanyika kwa njia bora, kugawa fedha hizo kulingana na mahitaji chini ya usimamizi wa wizara ya Elimu, utamaduni, maswala ya vijana na michezo inayoongozwa na waziri Francis Mathea.
"Pia tuna mswaada unaoitwa Nakuru County Persons with Disability Bill 2014 unaolenga kuwatetea zaidi walemavu, na pamoja na fedha hizo, walemavu watahisi hawajatengwa. Pesa hizo tutazipata hivi karibuni, pengine kabla ya mwaka ujao," aliongezea.
“Juhudi hizo ni za bunge nzima, si zangu pekee kwa sababu nilipowasilisha hoja hiyo bungeni wenzangu waliiunga mkono kwa dhati,” akasema Bi Emma.