Serikali ya kaunti ya Nyamira imetenga millioni 50 ambazo zitatoa ufadhili kwa wanafunzi na vijana wengine kujiendeleza kimasomo.
Pesa hizo zitawanufaisha wanafunzi wa familia maskini na mayatima kupata elimu ambayo itawasaidia nyakati zijazo.
Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Nyamira, Gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama alisema serikali yake tayari imeanzisha hazina kwa jina 'Ward Education Empowerment', ambapo 50 ,000,000 zimetengwa ili kufadhili wanafunzi kupata elimu.
“Serikali yangu inahitaji wale hawajiwezi kujiendeleza kielimu waweze kupata elimu katika shule mabalimbali ili nao wajisaidie siku za uzoni,” aisema Gavana Nyagarama.
“Kwa sasa tumetenga 50,000,000 na pesa hizo zitaenda kwa kila wadi ya kaunti hii ili kutoa ufadhili huo kwa wanafunzi kujiendeleza kimasomo,” aliongeza Nyagarama.
Pia benki ya KCB tawi la Nyamira ilitoa ufadhili kwa wanafunzi watano wa kaunti hiyo ambao hutoka familia maskini wanaojiunga na kidato cha kwanza mwaka huu ili kuendelea na masomo.
Kulingana na meneja wa benki ya KCB tawi la Nyamira Peterson Morara, walitoa shilling 300,000 kwa wanafuzi hao ili kuwagharamia mhula wa kwanza, huku akiahidi kuwa benki ya KCB itawasomesha wanafunzi hao hadi kidato cha nne.
“Tangu tuanze ufadhili huu mwaka wa 2012, tumesomesha wanafunzi 16 na tutaendelea hivyo hivyo, lengo letu ni kusaidia wanafunzi wale ni maskini kabisa kupata elimu,” alisema Morara.