Kaunti nane za North-Rift zimeungana pamoja kwa ajili ya kubuni mikakati ya pamoja kwa lengo la kuimarisha uchumi wa kanda hiyo.
Muungano huo unalenga kutafuta mbinu ya kuwezesha kaunti lengwa kunufaika kwa pamoja kutokana na mali asili ilioko katika maeneo hayo. Muungano huo wa kiuchumi unalenga kuleta pamoja kaunti za Nandi,Uasin Gishu, Trans Nzoia, Elgeyo/Marakwet, West Pokot, Baringo, Turkana na Samburu.
Kaimu mwenyekiti wa muungano huo gavana Jacksom Mandago alisema kila mkakati unawekwa ili kuona kwamba kila kaunti inanufaika pasipo kuegemea katika kaunti moja.
Mandago ambaye ni gavana wa kaunti ya Uasin-Gishu alisema muungano huo unatilia maanani uaminifu miongoni mwa kaunti wanachama ili kuhakikisha kuwa kila upande unanufaika kiuchumi.
Kupitia kwa waziri wa biashara katika kaunti ya Uasin-Gishu Philip Melly, Mandago aliondolea hofu ya kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa kaunti wanachama.
“Kile tunafanya kwa sasa ni kuendelea kutambua rasili mali katika kila kaunti kabla ya kuanza kutumia rasili mali husika kuboresha uchumi wetu kama kanda” alisema Bw Melly
Kwa mujibu wa Bw Melly ni kwamba muungano huo utatilia maanani shughuli za kiuchumi baina ya kaunti lengwa bila kuingiza siasa za mipaka ndani.
Tayari magavana kutoka kaunti hizo wanaendelea na misururu ya mikutano na warsha kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuhusu malengo nguzo hiyo ya uchumi North-Rift.
Kwa mujibu wa Bw Mandago ni kwamba kaunti zote wanachama zimeonyesha kuunga mkono mpango huo kwa dhati.
Kaunti ya Uasin-Gishu itakuwa mwenyeji wa warsha kuhusu uwekezaji katika kaunti hizo kama maandalizi ya kuzinduliwa kwa nguzo hiyo.
Warsha hiyo itaanza tarehe 18-21 mjini Eldoret.