Huenda kaunti za Pwani zikakosa kutimiza malengo ya ugatuzi iwapo sheria ya kuihusisha Jamii kuchangia katika mchakato mzima wa utoaji huduma za kaunti hautatumiwa vyema.
Msomi na mhadhiri wa Chuo kikuu cha Pwani mjini Kilifi Profesa Halim Shauri amesema kuwa lalama nyingi kutoka kwa jamii kuhusiana na utepetevu katika serikali za kaunti unatokana na hali ya viongozi kutowatambua wakazi.
Akizungumza katika kongamano la wasomi mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Shauri alisema kuwa hali inayoendelezwa na magavana na viongozi wengine wa kaunti za Pwani kuwabagua wakazi kamwe haifai, na lazima wakazi wahusishwe katika majadiliano muhimu ya kiuongozi na kimaendeleo mashinani.
Profesa Shauri amehoji kuwa ni lazima sheria hiyo ya kuwahusisha wakazi katika maamuzi yoyote ya kimaendeleo katika kaunti izingatiwe kwani imeangaziwa vyema kwenye katiba.
“Tunawahimiza viongozi kubadili mfumo wa uongozi wao na kuhakikisha kuwa masuala ya ugatuzi yanaangaziwa vyema ili kuhakikisha kuwa uongozi bora na maendeleo yanawafaidi wakaazi,” alisema Profesa Shauri.