Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika la kutetea maslahi ya wakongwe la Help Age International linataka kaunti zote nchini kutenga fedha za kuwasaidia wakongwe.

Shirika hilo lilisema hatua hiyo itasaidia kuboresha maisha ya wakongwe wengi ambao wanaishi maisha ya uchochole.

Mshirikishi wa shirika hilo Henry Neondo alisema juhudi zinazofanywa na serikali kuu kuwapa wakongwe shilingi 2,000 kwa mwezi hazijatosheleza wakongwe wote.

“Shilingi 2,000 ambazo serikali inatoa kwa wakongwe ambao wako na miaka zaidi ya 60 hazijafikia wakongwe wote hivyo basi kuna haja ya utawala wa kaunti kote nchini kuanzisha hazina kama hiyo ili kufikia wakongwe wengi mashinani,” alisema Neondo.

Akihutubu mjini Eldoret wakati wa mkutano wa viongozi wa mashirika ya kijamii kutoka North-Rift Neondo alisema hazina ya kitaifa ya kuwalipa wazee inafikia wazee 300,000 pekee ambayo alidai ni asilimia tano tu ya wazee waliohitimu kupokea fedha hizo.

Neondo aliongeza kuwa hazina hiyo itawasaidia wazee lengwa kumudu mahitaji yao ya kimsingi pamoja na kupata matibabu.

"Maisha magumu ambayo wazee wengi wanaishi husababisha vifo vya mapema miongoni mwa wakongwe," alisema.

Kiongozi huyo alitaka serikali kubuni sera ya kutoa matibabu spesheli kwa wakongwe katika hospitali zote za umma kote nchini.

Pia alitaka kuwe na vitengo spesheli vya kushughulikia afya ya wakongwe hospitalini ili wazee wasiwe wakipanga foleni hospitalini kama watu wengine.

Wakati huo huo kiongozi wa walio wachache katika bunge la kaunti ya Uasin Gishu Ramadhan Ali amesema atawasilisha hoja bungeni ya kuanzisha hazina ya wazee katika kaunti hiyo.