Share news tips with us here at Hivisasa

Kusikilizwa kwa kesi dhidi ya ‘Vampire’ wa Naivasha Geofrey Matheri, kulikosa kuendelea Ijumaa baada ya jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo kukosa kufika mahakamani.

Jaji Anthony Ndung’u aliyeskiza kwa muda pande husika kwa niaba ya jaji Maureen Odero, aliamrisha kesi hiyo isikilizwe wiki ijayo kwani jaji Maureen alikuwa na majukumu mengine ya kazi kwingineko, na kwamba yeye angeweza tu kupeana mwelekeo huo.

Mshukiwa Geoffrey Matheri kwa jina lingine la utani Fongo, ameshtakiwa kumdunga na kumfyonza damu Miriam Wairimu mnamo Agosti 29, 2008.

Wakati kesi hiyo ilisikilizwa hapo kabla, mahakama ilifahamishwa kwamba Matheri aliwazuilia wanawake wawili kwenye nyumba yake kama mateka, huku mashahidi wakisema waliona wanawake wawili waliokuwa dhaifu na walionekana kuumizwa.

Afisa mmoja wa polisi aliambia mahakama ya Naivasha kwamba, wawili hao walipatikana katika nyumba ya mshukiwa aliyelaumiwa kwa kuua wanawake na kuwafyonza damu.

Kwa sasa Matheri anayeshtakiwa pia kwa kumuua Miriam Wairimu, amo kizuizini.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa mnamo tarehe 26, November.