Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mahakama kuu ya Nakuru Ijumaa iliwaamuru walishaji mifugo wawili wanaodaiwa waliwapa sumu simba wanane waendelee kukaa ndani hadi ombi la kufutilia dhamana ya Sh2 milioni isikizwe na kuamuliwa.

Simindei Naururi na Kulangash Toposat wameshtakiwa kuwapa sumu Simba hao wanane katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara.

Naururi na Toposat walishtakiwa Desemba 23, 2015 katika mahakama ya Narok na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni na hakimu mkazi Bw Allan Sitati.

Jaji James Wakiaga alisitisha agizo la Sitati la kuachiliwa kwa wachungaji hao hadi ombi lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Wakiaga aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura.

Naururi na Toposat wanashtakiwa kwa kosa la kuwapa sumu wanyama pori na kuhatarisha Simba.

Kesi hiyo itatajwa katika mahakama ya Nakuru Januari 13.