Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwanasheria mkuu hana wajibu wa kuhakikisha kwamba mpango wa serikali ya kitaifa wa kuboresha uchumi unatekelezwa na haswaa katika kuhakikisha wauguzi walio chini ya mkataba wanapata ajira ya kudumu.

Hilo limesemwa mahakamani na mwendesha mashtaka wa serikali Nguyo Wachira aliyekuwa akimwakilisha mwanasheria mkuu katika kesi ambayo imewasilishwa kwenye mahakama ya Nakuru inayohusiana na maswala ya leba na uajiri.

Akizungumza siku ya Jumanne, Wachira aidha alihoji kuwa serikali za kaunti zinafaa kutafuta idhini ya wizara ya fedha pamoja na fedha za kuziwezesha kuwajumuisha wauguzi hao kupitia kwa bodi husika.

Izingatiwe kuwa muungano wa kitaifa wa wauguzi umewasilisha kesi mahakamani dhidi ya baraza la magavana, tume ya huduma za umma, wizara ya afya pamoja na kaunti tano ukidai wauguzi ambao wako chini ya mkataba wanafaa kupewa ajira ya kudumu na serikali za kaunti.

Katika kesi hiyo, iliyowasilishwa mahakamani mapema mwaka huu, muungano huo wa wauguzi ulidai kwamba kaunti zilibadili yaliyomo kwenye mpango wa serikali ya kitaifa wa kuboresha uchumi baada ya kuongeza mkataba wa wauguzi walio chini ya mkataba kwa muda wa miezi sita mnamo mwezi Mei mwaka wa 2014, na hatua hiyo huenda ikawapelekea wauguzi hao kukosa ajira huku muda unapoyoyoma.

Wauguzi hao walikuwa wamepewa ajira ya muda mwaka wa 2011 chini ya mkataba wa miaka mitatu na serikali ya kitaifa na kwa sasa wanataka kuwepo kwa makubaliano baina ya kaunti hizo tano ili waweze kupata ajira ya kudumu chini ya kaunti hizo.

Mikataba hiyo ya wauguzi walio chini ya kaunti za Siaya, Baringo, Transzoia na Narok zilifaa zifikie tamati mnamo mwezi Mei mwaka wa 2014, lakini ilirefushwa kwa muda wa miezi sita.

Ni muhimu kuashiria hapa kuwa baraza la magavana limekataa kujihusisha na majadiliano kuhusiana na hatua ya kuwapa ajira ya kudumu wauguzi hao likisema kuwa wauguzi hawaaajiri na kaunti .

Kesi hiyo itaendelea mwaka ujao.