Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Muungano wa wakimbizi wa ndani kwa ndani Kenya-Kidipo, sasa unaitaka serikali kutombagua mkimbizi yeyote wakati wa kuwapa makao wakimbizi waliosalia nchini, katika awamu inayotarajiwa kung’oa nanga Februari 15, 2016.

Wakiongea Alhamisi mjini Nakuru, vinara wa muungano huo wamesema wanapania kuimarisha amani na umoja miongoni mwa Wakenya wa tabaka zote nchini.

Walisema wakati umefika ambapo Wakenya wanafaa kukataa kugawanywa kikabila na kukumbatia amani licha ya yaliyoshuhudiwa mwaka wa 2007.

Mwenyekiti wao Peter Tena alisema ombi lao kama wakimbizi ni kuona serikali ikifanya kazi hiyo bila kushurutishwa ama mapendeleo.

“Tuna ujumbe kutoka kwa serikali kwa wenzetu ambao ni wakimbizi wasio na mashamba, serikali inapania kuanza zoezi hilo februari 15, na tunaomba liwe la huru na haki,” alisema Peter Tena.

Wakati uo huo amewaonya wakimbizi dhidi ya kuchochewa na wanasiasa walio na nia zao za kibinafsi katika kuzozana na serikali.

“Wakimbizi hawafai kuchochewa na watu kutoka idara fulani za serikali kuandamana kama ilivyofanyika jana Gilgil,” alisema Tena.

Muungano huo umesema kuwa una imani na mawaziri wapya chini ya serikali ya Jubilee haswa wizara ya ugatuzi, kuwa watawapa makao hivi karibuni.