Spika wa bunge la kaunti ya Nakuru Susan Kihika amehimiza hazina ya kitaifa kuongeza kiwango cha fedha kinachotolewa kila mwezi kwa wakongwe na watu walio na ulemavu.
Anasema hatua hiyo itasaidia katika harakati za kuhakikisha kwamba wote wanaolengwa kuafikiwa kwenye mpango huo wanafaidika.
Akizungumza mjini Gilgil Alhamisi tarehe 17 alipotoa msaada kwa wakongwe na watu walio na ulemavu, Kihika alisema kwamba kiwango cha fedha kinachowafikia watu hao ni kidogo mno huku watu wengi wakikosa kujumuishwa kwenye mpango huo.
"Tunapozunguka kwenye maeneo mbalimbali, ninajihisi kuwa kama spika wa bunge la kaunti ya Nakuru, wajibu wangu hauishii hapo. Najihisi nina wajibu wa kuwasha mshumaa ninapoona kuna giza. Kile ambacho nimegundua haswaa mwaka huu ambapo nimepata kujumuika na wakongwe ni kwamba fedha ambazo zimetengwa kwa minaajili ya kuwasaidia wakongwe na walio na ulemavu hazitoshi na kwa wakati mwingine, fedha hizo haziwafikii wale ambao wanalengwa kwenye mpango huo," alidokeza Kihika.
Kulingana na Kihika, fedha hizo pia zinafaa kuongezwa ili ziwaweze kuwasaidia pakubwa walio na ulemavu na wale wakongwe kwani wengine wanahitaji kununua dawa pamoja na vyakula maalum.
"Natumai kwamba wote wanaolengwa na fedha hizo watafikiwa ili kwamba wale wanaolengwa na fedha hizo waweze kutosheleza mahitaji kama vile kununua dawa wanazohitaji na pia chakula," aliongeza Kihika.
Katika kuweza kuwasaidia walio na ulemavu na wale wakongwe kuafikia mahitaji hayo, Kihika amearifu kuwa serikali ya kaunti ya Nakuru imeweza kupitisha hazina ya shilingi millioni 55 akisema kila wadi iliyo chini ya kanti ya Nakuru itatengewa shilingi milioni moja kwenye fedha hizo.
Hivyo basi, amewataka wale wanaolengwa kwenye fedha hizo kujitokeza na kujisajili ili waweze kunufaika na fedha hizo.
“Kwenye kaunti, tuna aina ya watu walio na ulemavu na wajibu wangu ninapozuru maeneo mbalimbali wakati huu wa krismasi ni kuwahimiza walio na ulemavu kujitokeza na kujisajili. Waliotwikwa jukumu hilo kwenye wadi lazima wahakikishe idadi yao yajulikana. Kama serikali ya kaunti tuna sheria kwamba shilingi milioni moja inatengewa kila wadi ili wale wanaoishi na ulamavu waweze kufaidika," alisema Kihika.