Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa eneo la Pwani wameshauriwa kujiepusha na watu wenye nia ya kuvuruga amani msimu huu wa sherehe za krismas na mwaka mpya.

Mshirikishi Mkuu wa serikali na Utawala katika eneo la Pwani Samuel Kilele alilitaja suala zima la ukosefu wa usalama kuwa changamoto kuu kwa wakazi wa eneo hilo.

Kilele alionya kumchukulia hatua kali za kisheria yeyote atakayepatikana akivuruga amani huku akihimiza maafisa wa usalama kuwajibikia majukumu yao ipasavyo wakati huu.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Kilele alisema kwamba uhaba wa maafisa wa usalama na utawala kushughulikia masuala mbali mbali ya jamii kumechangia kukithiri kwa magenge ya wahalifu na lazima yakabiliwe.

Aidha, aliwataka wakazi kuwa katika mstari wa mbele kuwaripoti washukiwa wa uhalifu na wale wanapanga njama ya kuvuruga usalama ili kutiwa nguvuni na maafisa wa usalama.

“Tunawaonya wale wanaolenga kuvuruga amani wakati huu wa msimu wa sherehe kukoma mara moja maana maafisa wa usalama wako macho na kukabiliana nao kikamilifu,” alisema Kilele.