Siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumtaka papa mtakatifu Francis kumwombea alipokuwa hapa nchini katika ziara yake ya Afrika, mbunge mmoja kutoka Nakuru ametilia mkazo haja ya maombi kwa nchi.
Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amesema rais na naibu wake wanahitaji maombi na ushirikiano wa wakenya ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikumba serikali kama ufisadi.
Akiongea katika mkutano na walemavu wa eneo bunge lake katika wadi ya Kiamaina, Kimani alisema kwamba ufisadi hauna nafasi katika serikali ya Jubilee, ndio maana Uhuru akawatema mawaziri walioshukiwa kuhusika na ufisadi.
“Rais alipoteua mawaziri hakuwarudisha wale waliojiuzulu kwa sababu ya kashfa za ufisadi, hiyo ina maana atahakikisha ufisadi unaorudisha uchumi wetu nyuma umekomeshwa,” alisema Kimani.
Wakati uo huo, Kimani alisifia uhusiano mwema kati yake na spika wa bunge la kaunti ya Nakuru Susan Kihika, huku akisema sasa wamo kwenye ‘meli moja’ ya kisiasa.
Wiki jana katika hafla ya kuchangisha pesa kwenye kanisa la PCEA eneo la Workers, Kimani alitangaza kuzika tofauti zake za kisiasa na spika ambaye pia alikuwako.
Katika taarifa kwa wanahabari, Joe Ngugi, ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano katika ofisi ya mbunge Ngunjiri , alisema: “Bi Kihika na mheshimiwa Kimani wamegundua kwamba tofauti zao za kisiasa zinarudisha maendeleo nyuma, na wameamua kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi ya maendeleo”.