Wanawake kutoka kaunti ya Nyamira wameombwa kupimwa ili kujua hali ya ukimwi na magonjwa ya saratani ya matiti na uzazi kama njia moja ya kuwahakikishia afya yao.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Haya ni kulingana na mwenyekiti wa kamati ya kuthibiti virusi vya ukimwi katika kaunti hiyo Rachael Nyaboke, aliyekuwa akiwahutubia kina mama katika eneo la Nyakenama katika kaunti ndogo ya Nyamira kaskazini. 

"Yafaa kina mama kujua hali yao, kwa hivyo ni sharti mvitembelee vituo vya afya ili kupimwa na kujua hali zenu mapema," alisema Nyaboke. 

Nyaboke aidha aliwahimiza kina mama kuepuka tabia za kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa ili kusaidia katika kuthibiti visa vya maambukizi. 

"Ni furaha kujua kuwa baadhi ya kina mama hujitokeza kupimwa, ila tunahitaji wengine zaidi kujitokeza kupimwa iwapo wameathirika na virusi vya ukimwi kwa kuwa virusi hivyo vinaweza vikawa mwilini kwa miaka kumi bila ya kugunduliwa," aliongezea Nyaboke.