Mbunge wa Changamwe Omari Mwinyi amewahimiza kina mama mjini Mombasa kukoma kukaa na kuwategemea waume wao kwa mahitaji ya kila siku, na badala yake wajitokeze na kushiriki kazi za mkono kama kina mama wa sehemu zingine.
Akizungumza siku ya Jumanne alipozuru eneo la ujenzi wa reli wa kisasa maarufu kama 'Standard Gauge Railway' unaendelea, Mwinyi alidai kukerwa na idadi ndogo ya wanawake waliojitokeza kushiriki shughuli hiyo ikilinganishwa na maeneo mengine.
‘’Kina mama wetu hawapendi kazi za mkono, badala ya kujitokeza hapa kwa wingi na kushiriki ujenzi huu ili kupata pesa wanasalia tu majumbani,’’ alisema Mwinyi.
Mwinyi vilevile aliwaahidi wavuvi wanaovua katika sehemu za Mwangala, Kume, Mkute na Mtongwe kuwa atazungumza na mwenyekiti wa tume ya ardhi nchini Muhammad Swazuri ili kuhakikisha kuwa wanafidiwa kabla maeneo hayo kuzibwa kutoa nafasi ya kwa ujenzi wa reli hiyo.
Mapema mwezi huu, wavuvi takribani 1,500 wanaotegemea bahara hizo waliandamana huku wakiilaumu tume ya ardhi nchini kwa kile walikitaja kama kupuuzwa na tume hiyo kufuatia kucheleweshwa kwa fidia waliyoahidiwa na serikali.