Kina mama katika kaunti ya Nakuru wametakiwa kuwaunga mkono kina mama wenzao watakaowania viti vya uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
Mwaniajikiti cha uakilishi wadi cha Kiamaina Rachael Wanjohi amesema kuwa kina mama wanaweza kushinda viti vingi sana iwapo wataungwa na kupigiwa kura na kina mama wenzao.
Akiongea Jumanne alipotoa mchango wa vifaa vya kutengeneza nywele kwa kikundi kiomja cha kina mama mtani mailisita, Bi Wanjohi alisema kuwa uadui kati ya kina mama ni kizingiti kikubwa kwao kuingia uongozini.
“Idadi ya wanawake katika taifa hili ni kubwa kushinda ya wanaume lakini wanaume ndio wanaotawala uongozi na hii ni kwa sababu sisi kina mama tumekataa kuwaunga mkono wenzetu sababu ya chuki," alisema Wanjohi.
Alisema kuwa itakuwa vigumu kwa shida ya kina mama kutatuliwa iwapo hawataungana na kuingia uongozini.
“Kama tunataka shida zetu zitatuliwe basi itatulazimu tushikane wakati wa uchaguzi na tuwatume kina mama wengi katika bunge la kaunti na hata kule Nairobi,” aliendelea kusema.
Aidha aliwataka kina mama kujitokeza na kupiganaia nafasi za uongozi wakati wa uchaguzi na kuwataka wanasiasa wanaume kuwaheshimu kina mama wanaopiganaia viti.
“Vyama vya siasa na wanaume wanapaswa kutuheshimu sisi kina mama na wawache kutuona kama watu dhaifu wasioweza kuongoza,” aliongeza.