Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya afya ya umma katika Kaunti ya Nakuru inanuia kuwapa idadi kubwa ya watoto chanjo ya polio licha ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Akizungumza Mjini Nakuru siku ya Jumanne, afisa msimamizi wa maswala ya afya katika Kaunti ya Nakuru Samuel King’ori, alisema kuwa shughuli hiyo ya kuwachanja watoto inaendelea pasi na vikwazo vyovyote.

“Tunalenga kuwapa chanjo watoto wasiopungua 394,687,” alisema King’ori.

Afisa huyo alidokeza kuwa kaunti ndogo ya Nakuru Mashariki inaongoza kwa asilimia 77 ya watoto waliopewa chanjo hiyo, na kufuatwa na eneo la Gilgil kwa asilimia 64.

Maeneo mengine ni kama vile Nakuru Kaskazini- asilimia 61, Molo- asilimia 58, huku eneo la Naivasha likiwa la mwisho na asilimia 57.

King’ori alisema kuwa mvua kubwa inayoendelea kunyesha mjini Naivasha pamoja na ukosefu wa miundo msingi bora imefanya shughuli hiyo kuwa ngumu.

Msimamizi wa maswala ya afya wilayani Naivasha Dkt Oren Ombiro, amesema kuwa maeneo ya Kirima, Kwa Wangu, Maella na Kongoni hayapitiki kutokana na ubovu wa barabara.