Kiongozi wa Mombasa Republican Council (MRC) amefunguliwa mashtaka matatu yakiwemo kuwa mwanachama wa kundi lililopigwa marufuku.
Shitaka la pili ni kupokea na kuchangisha shilingi elfu 210 pesa taslim zinazoaminika kuwa za kufadhili kundi la MRC, huku shtaka la tatu ni kuwa na stakabadhi zilizokuwa na maandishi ya “Pwani si Kenya”, maandishi yaliyotajwa kuwa ya uchochezi.
Kiongozi huyo, Omar Mwamnuadzi, alikanusha mashtaka yote matatu siku ya Jumatatu mbele ya Hakimu Mkaazi Paul Mutai.
Hakimu Mutai, aliagiza mshtakiwa huyo kuzuiliwa kwa siku tano katika Kituo cha polisi cha Kwale ili kutoa nafasi kwa upande wa mashtaka kufanya uchunguzi wa kesi hiyo.
Hatua hii inajiri baada ya upande wa mashtaka kuomba kupewa siku saba ili kukamilisha uchunguzi wa kesi hiyo.
Mwamnuadzi alikamatwa siku ya Jumapili na maafisa wa polisi nyumbani kwakem eneo la Ng’ombeni.
Kesi yake itatajwa Januari 29, 2016.