Kiongozi wa vijana katika wadi ya Kivumbini, Nakuru Martin Lunalo amehofia maisha yake kwa kile anadai ni kuhangaishwa na watu anaowaita maadui wa maendeleo.
Akiwahutubia wanahabari Jumatatu, Lunalo anasema kuwa juhudi zake za kuwafunza vijana kuhusu katiba na haki zao eneo hilo ndilo limechangia baadhi ya viongozi kuanza kumtishia maisha.
"Mimi nafunza tu vijana mambo ya katiba lakini sasa baadhi ya viongozi ambao hawataki vijana waelewe katiba na hata kuongoza wanapinga," alisema Lunalo.
Lunalo anasema kuwa aliwai lazimishwa kulala makaburi ya Nakuru kusini akitakiwa kueleza anakotoa fedha za kuelimisha vijana, lakini hatua hiyo haijamtia wasiwasi.
Amesema kuwa kando na vitisho hivyo, hatakufa moyo bali atazidi kuwaelimisha vijana wa Kivumbini kuhusu maslahi yao na haki za kikatiba.