Hatimaye mpango wa kuezeka kituo cha uzalishaji nguvu za umeme kupitia jua almaarufu 'solar energy' kule Sironga, kaunti ya Nyamira umeidhinishwa na kamati ya washikadao mbalimbali. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia wanahabari baada ya mkutano huo uliohuzisha kampuni ya utoaji ushauri Vatek kwenye mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Jumatano, waziri wa mazingira, maji na mali asili Kepha Osoro alisema serikali ya kaunti hiyo itatia sahihi ya makubaliano ya ununuzi wa nguvu za umeme pamoja na kampuni ya uzalishaji nguvu za umeme nchini KENGEN. 

"Tutatia sahii ya makubaliano na kampuni ya Kengen ili tuiuzie nguvu za umeme tutakaozalisha ili kwamba Kengen iuzie kampuni ya usambazaji umeme nchini," alisema Osoro. 

Waziri Osoro amesema mradi huo utakaogharimu shillingi billioni 7.5 tayari umetengewa kipande cha ardhi chenye hekari 400 kule Sironga.

"Tumetenga kipande cha ardhi chenye hekari 400 kule Sironga kwa minajili ya kuezeka mradi huo utakaozalisha megawatt 50 za stima ili kwamba mradi huo uwasaidie wakazi wa kaunti hii kuimarisha maisha yao kiuchumi," aliongezea Osoro. 

Mradi huo ni moja ya miradi aliyoahidi kuitekeleza gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama miaka miwili iliyopita.