Mbunge wa Njoro Joseph Kiuna anataka umri unaoruhusiwa kwa watu kunywa vileo kubadilishwa kutoka miaka 18.
Hatua ya Kiuna inaunga mkono takwa la mwenyekiti wa NACADA John Mututho ambaye pia anataka umri huo ubadilishwe kutoka miaka 18 hadi miaka 21.
Kiuna alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza maafa ya vijana wanaojiingiza katika anasa za unywaji wa pombe akiangazia kisa cha vijana watano walioaga dunia kwenye ajali ya barabarani katika eneo la Salgaa. Vijana hao walifariki mkesha wa kuamkia mwaka wa 2016 baada yao kudaiwa kubugia vileo na kuendesha gari.
Akiongea eneo la Kikapu huko Njoro , Kiuna alisisitiza kuwa ajali za mara kwa mara zinazotokea kwenye eneo la Salgaa zinaweza kukomeshwa kupitia sheria muhimu.
Kiuna alisema suluhu la ajali ambazo zinashuhudiwa eneo hilo la Salgaa linafaa kutafutwa na viongozi mara moja.