Wakulima wa chai  wanaopeleka mazao yao kwenye kiwanda cha kusaga majani chai cha Nyansiongo sasa wana kila sababu ya kutabasamu, baada ya usimamizi wa kiwanda hicho kukubali kukumbatia mbinu mpya za kuimarisha uzalishaji. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye kiwanda hicho siku ya Jumatano, mwenyekiti wa kiwanda cha Nyansiongo Peter Nyakora alisema kuwa kiwanda hicho sasa kitakuwa kikiwaruhusu wakulima kupokea mbolea mara mbili kwa mwaka na pia kuwatuma wataalamu wa kilimo kutembelea wakulima wanaokuza zao hilo la chai ili kuwapa ushauri jinsi yakuimarisha kilimo cha chai.

"Nina furaha kuwafahamisha kuwa kuanzia sasa usimamizi wa kiwanda hiki utaanza kuwapokeza wakulima mbolea mara mbili kwa mwaka kuanzia Januari mwakani na pia tutawatuma wataalamu mbalimbali kutembelea wakulima wanaokuza chai ili kuwapa ushauri jinsi ya kuimarisha kilimo cha ukuzaji chai," alisema Nyakora. 

Nyakora aliongeza kwa kusema kuwa usimamizi wa kiwanda cha Nyansiongo utaanzisha warsha za kuwapa mafunzo wakulima juu ya kuimarisha kilimo cha ukuzaji chai, akiongezea kuwa huenda kampuni hiyo ikaanza kuwazawadi wakulima bora kama njia mojawapo ya kuwapa motisha. 

"Tutaanza kufanya warsha kwa wakulima ili kuhimizana jinsi ya kuimarisha kilimo cha ukuzaji chai na tuanaendelea kudadisi swala la kuwazawadi wakulima bora ili kuwahimiza wengine kutia bidii zaidi," alisema Nyakora. 

Haya yanajiri baada ya kamati kuteuliwa kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuimarisha uzalishaji miongoni mwa wakulima.