Kulishuhudiwa vioja katika kivuko cha feri cha Likoni Jumatatu asubuhi baada ya watu kadha kuanguka na kupata majeraha madogomadogo kufuatia utelezi ambao umesababishwa na mvua nyingi ambayo imekuwa ikinyesha tangu usiku wa Jumapili.
Wanane hao walijipata katika masaibu hayo baada ya umati ambao ulikuwa umeanza kuleta fujo kuruka kuta za mabanda na kukimbilia feri ambazo zilikuwa zimechelewa kufika kwa wakati ufaao ili kuwavusha kwa madai kuwa kulikuwa na meli ambayo ilikuwa inapita.
Hata hivyo ilikuwa vibaya zaidi kwa mkazi mmoja, Michael Mute, ambaye alianguka na kuumia mikono na kichwa, na kupoteza baadhi ya hati zake.
Hata hivyo, baadhi ya hati zake ambazo zilikuwa tayari zimeingia baharini ziliweza kuokolewa na mpiga mbizi mmoja ambaye alijitolea kuokoa jahazi.
Wengi wa wakazi walilaumu shirika hilo kwa kuendelea kuwanyanyasa wakazi kutoka pande za Likoni pamoja na kuwaweka wateja wa magari kwa muda mrefu kwenye msongamano wa magari.
Kulingana na abiria mmoja, mkurugenzi wa shirika hilo ameamua kupuuza maoni ya wakazi ya kuhakikisha kuwa kuna feri nne zinazohudumu hasa nyakati za asubuhi na jioni wakati ambao kunashuhudiwa idadi kubwa ya watu na magari.
Wengi wao walisema kuwa hadi mkurugenzi atakapong’atuka mamlakani ndio shughuli zitakuwa sawa, na huenda shida kubwa ikatokea iwapo serikali ya taifa itaendelea kuzembea bila kutilia maanani maslahi ya umma.