Share news tips with us here at Hivisasa

Kizazaa kilizuka mapema Ijumaa katika shule ya msingi Nyakiambi iliyoko eneo la Elburgon kaunti ya Nakuru baada ya wazazi kuvamia shule hiyo na kupinga hatua ya mwalimu mkuu ya kuwafurusha wanafunzi nyumbani kwa kosa la kukosa kulipa shilingi 200 ya kugharamia ziara ya walimu hadi mjini Mombasa.

Aidha wazazi hao waliojawa na gadhabu walijitwika jukumua la kuwaamuru wanafunzi wote kwenda nyumbani bila kutaka kumpa fursa mwalimu mkuu Allan Mbugua aliyejaribu kutuliza hali hiyo wakimtaja kama aliyefanya hatua hiyo bila kuwahusisha.

Kulingana na walimu walioongea na vyombo vya habari walisema kuwa awali walifahamishwa kuwa shilingi 150 ilikuwa inagharamia ziara hiyo iliyotokana na kuimarika kwa matokeo yao ya mitihani huku shilingi 50 zilizosalia ikilengwa kusaidia mtoto aliyepata alama 315 na kufanikiwa kujiunga na shule ya upili ya Koelel, Gilgil na anatoka familia isiyojiweza.

Hata hivyo wazazi hao walimtaja mwalimu mkuu kama aliyeanza mtindo wa kuitisha hela kwa lengo fulani la shule na kisha baadaye hela hizo kupotea kwa njia isiyoeleweka.

“Tunataka waziri Matiang’i aingilie kati maanake huyu mwalimu mkuu anatuhadaa,” wazazi hao walisema.

Kwa upande wake mwalimu huyo mkuu alisema kuwa hatua yake imetokana na uamuzi wa wazazi 120 wakati wa kikao cha kurudisha shukrani kwa matokeo bora ya shule hiyo ya mwaka huu.