Share news tips with us here at Hivisasa

Hatima ya wanafunzi 122 wa Kaunti ya Kilifi kujiunga na vyuo vikuu haijabainika baada ya Baraza la Mitihani Nchini (Knec) kufutilia mbali matokeo yao ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne kufuatia madai kuwa walihusika na visa vya udanganyifu.

Kati ya shule zilizoathirika ni ile ya Upili ya Arabuko Forest ikiwa na wanafunzi 46, Kilifi Private 36, Barani 31 huku majibu ya wanafunzi 9 wa Shule ya Upili ya St Johns yakiwa yamezuiliwa kutokana na utata wa vyeti vya kuzaliwa.

Mkurugenzi mkuu wa Elimu Kaunti ya Kilifi, Dickson Ole Keis, alisema licha ya kufutiliwa mbali kwa matokeo ya wanafunzi hao, kaunti hiyo imeimarisha viwango vya matokeo kwani imepata alama wastani ya 4.26 ikilinganisha na 4.16 ya mwaka wa 2014.

“Japo matokeo ya zaidi ya wanafunzi 122 hajabainika hatima yake kutokana na kuwa bado yanazuliwa na baraza la mitihani nchini kwamba huenda wakawa walihusika na udanganyifu wa mitihani ya kitaifa KCSE, kaunti ya Kilifi imejaribu tena sana kwani imepata alam wastani ya 4.26,” alisema Keis siku ya Ijumaa katika mkutano wa elimu na walimu wakuu.

Kaunti Ndogo za Magarini, Kaloleni na Malindi zimefanya vyema zaidi kuliko zile za Ganze, Rabai na Kilifi.