Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa vyama vya kutetea maslahi ya walimu nchini KNUT na KUPPET katika kaunti ya Mombasa wamepinga vikali zoezi la kutia saini kandarasi ya utendakazi wakisema kuwa linalenga kuwakandamiza walimu.

Wakiongea mjini Mombasa siku ya Jumanne baada ya kukamilika kwa kongamano la kusisitiza shughuli hiyo lililoandaliwa na Tume ya kutathimini mishahara ya wafanyikazi wa umma SRC, viongozi hao walisema kuwa mpango huo ni njama ya serikali kukwepa kuwalipa walimu marupurupu yao.

Akiwahutubia walimu baada ya kungamano hilo, katibu wa chama cha KNUT katika kaunti ya Mombasa Dan Aloo alisema kuwa hatua hiyo huenda ikavuruga mpango wa kuboresha sekta ya elimu nchini, na iwapo serikali inataka walimu kukubali mpango huo basi lazima walipe walimu ahadi yao ya asilimia 50 na 60 wanayodai serikali.

"Tunawaambia SRC kuwa kamwe hatutakubali mpango wao wa kutia saini kandarasi ya utendakazi kutokana na kuwa wana njama ya kuwakandamiza walimu, ikiwa wanataka tukubaliane na mpango huo, basi kwanza watupe ahadi yetu ya asilimia 50 na 60 ya marupurupu na nyongeza ya mishahara ya walimu tunayodai," alisema Aloo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa tume ya SRC Sara Serem kupitia ujumbe wake uliosomwa na Naibu Mkurugenzi wa Tume hiyo David Muthaka ameeleza kuwa mpango huo unalenga kuimarisha utendakazi bora katika sekta ya elimu.

Katibu wa chama cha KNUT katika kaunti ya Mombasa Dan Aloo akiwahutubia walimu kuhusiana na swala la kandarasi ya utendakazi mjini Mombasa.