Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu wa chama cha Kutetea maslahi ya walimu Knut katika Kaunti ya Mombasa Dan Aloo ameukosoa mpango wa Tume ya kuajiri walimu nchini TSC wa kutaka walimu kutia saini kandarasi za utendakazi kwa madai kuwa shughuli hiyo itasaidia tume hiyo kuwapandisha vyeo walimu waajibikaji.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu baada ya kuhudhuria kongamano la walimu, wadau wa sekta ya walimu pamoja na makamishna wa tume hiyo, Aloo alisema kuwa makamishna hao wangefaa kujadiliana na viongozi wakuu wa chama hicho kabla ya kuwafikia walimu.

Alisema kuwa kamwe walimu hawatakubali mpango huo hadi vipengele vya tume hiyo kurekebishwa na tume hiyo kujadiliana vyema na walimu pamoja na kutatua suala tata linalowazonga walimu la nyongeza ya mishahara na marupurupu yao ya asilimia 50 na 60.

“Tunawaambia makamishna wa TSC kujadiliana kwa kina na viongozi wakuu wa chama chetu cha Knut pamoja na kutatua shida tuliyo nayo ya tangu jadi ya nyongeza ya mshahara na marupurupu tuliyoitisha kabla hawajatuambia mipango waliyo nayo,” alisema Aloo.

Kauli ya Aloo imejiri huku tume ya TSC ikishikilia kuwa lazima walimu kutia saini kandarasi hiyo iwapo wanahitaji kazi la sivyo tume hiyo iajiri walimu wengine zaidi nchini.