Viongozi wa Chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini Knut sasa wameitaka Wizara ya Elimu nchini pamoja na Baraza la Mitihani Knec kueleza wazi kilishosababisha kukithiri wa maswala ya udanganifu wa mitihani ya kitaifa.
Katibu wa chama hicho katika kaunti ya Mombasa Dan Aloo, alisema kuwa sekta hizo mbili ndizo zilizosababisha kuchipuka kwa maswala ya udanganyifu wa mitihani ya kitaifa ya KCSE wa mwaka wa 2015.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi baada ya matokeo ya mitihani ya kitaifa ya KCSE kutangazwa na Wiziri wa Elimu nchini Dkt Fred Matiang'i katika jumba la mtihani jijini Nairobi, Aloo alisema kuwa zaidi ya wanafunzi 5,000 huenda wakakosa matokeo yao ya mitihani ya kitaifa baada ya baraza hilo kusema kuwa wanafunzi hao walihusika katika udanganyifu wa mitihani.
Alisema kuwa hatua hiyo inamnyima fursa mwanafunzi kusonga mbele kimasomo pamoja na kudidimiza ndoto yake katika siku za usoni kwani itamlazimu kurejea shuleni ili kuendeleza masomo yake katika nafasi ya vyuo vikuu.
“Tunaitaka Wizara ya Elimu nchini pamoja na baraza la mitihani nchini Knec kueleza bayana chanzo kikuu kilichosababisha wanafunzi kuhusika katika udanganyifu wa mitihani kwani sekta hizo mbili zilizembea wakati wa kusambaza mitihani shuleni,” alisema Aloo.
Kauli ya Aloo inajiri baada ya Waziri wa Elimu nchini Dkt Fred Matiang'i kutangaza kuwa zaidi ya wanafunzi elfu tano watakosa majibu yao ya mitihani ya kitaifa ya mwaka wa 2015.