Kufuatia kampeni za uchaguzi wa maafisa wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini Knut kuendelea kupamba moto katika maeneo mengi katika Kaunti ya Nyamira, naibu katibu wa eneo hilo anayeondoka James Oteki amejitokeza kuwahimiza walimu kuwa watulivu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu siku ya Jumanne, Oteki aliwahimiza wagombezi wa nyadhifa mbalimbali kuendesha kampeni zao kwa amani na umoja, huku wakizingatia sheria ili uwazi kushuhudiwa wakati wa uchaguzi. 

"Kuwa na uchaguzi chamani ni ishara wazi kwamba tunazingatia demokrasia, na kamwe hilo halimaanishi kuwa sharti uadui ushuhudiwe kati yetu na hili ni zoezi litakalodumu kwa mwezi mmoja tu, na ndio maana lazima tuwe kitu kimoja ili kupambana na maadui wetu," alisema Oteki. 

Kwa upande wake katibu wa chama hicho tawi la Masaba Meshack Ombongi aliongeza kwa kuwahimiza wagombezi wa nyadhifa mbalimbali kuzingatia uwazi kwenye zoezi hilo.

"Sisi walimu ni kioo cha jamii na sharti tuongoze kwa mfano mwema, na ndio maana inahitajika kwamba wanasiasa wanastahili kuiga uwazi kutoka kwetu na ndio maana sio bora kuwahonga walimu ili kutupia kura kama viongozi kwa maaana hiyo ni njia mojawapo ya kuangamiza demokrasia baina yetu," aliongezea Ombongi.