Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa zamani wa Subukia Koigi wa Wamwere, amekiri kwamba idara ya mahakama JSC haina uwezo tena wa kurejesha imani yake kwa Wakenya, kutokana na jinsi imevaamiwa na “kirusi cha ufisadi.”

Koigi akizungumza katika redio moja ya Nakuru iitwayo Sauti ya Mwananchi, Jumamosi jioni, pia aliitaka tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, ijiuzulu na kupisha kuteuliwa kwa tume nyingine itakayohakikisha uchaguzi wa 2017 utakuwa huru na wa haki.

Mwanasiasa huyo alisema kwamba JSC na IEBC ndizo taasisi ambazo zinawapa Wakenya haki katika uchaguzi na kutatua mizozo ya uchaguzi, lakini hazina uwezo wa kufanya hivyo katika uchaguzi mkuu ujao, baada ya kuvaamiwa na ufisadi.

“Zamani tuliskia mahakimu wanahongwa, lakini sasa madai yameibuka ya majaji wa mahakama za juu kujihusisha katika ulaji rushwa, na kuendekeza ufisadi ili kupendelea mgombea fulani katika uchaguzi. Idara kama hiyo ni ya kutegemewa kweli?” alihoji Koigi.

Aidha alisema: “IEBC ifunge virago vyake, na iende nyumbani, sina imani nayo pia, kwa sababu inashukiwa ufisadi wa Chikengate.”

Mchanganuzi huyo alisema ili kuzuia mafarakano ambayo yanaweza kutokea baada ya uchaguzi, ni lazima tasisi hizo mbili ziwe zinaaminika na pande zote mbili, upinzani na serikali.

“Ikiwa serikali au mbunge au afisa yeyote yule atatetea tume ya uchaguzi, ni kumaanisha anaungana nayo mkono katika utedakazi wake, na vile vile akipinga, ni kumaanisha kuna jambo analohofia. Kwa hivyo IEBC ijiweke kama ilivyo; tume huru, ambayo haipendelei upande wowote iwe upinzani ama serikali, na njia ya kufanya hivyo ni kwa kuhakikisha haijaongozwa na umero, ulafi na hongo kutoka pande zote mbili,” akasema Koigi.