Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Waziri wa kawi Charles Keter amelitaka shirika la usambazaji umeme nchini KPLC, kuhakikisha kwamba limekamilisha kazi ya kuweka stima katika shule zote za msingi nchini chini ya muda uliotolewa, ambao unatamatika Jumamosi 20, Feb, 2016.

Akizungumza kwenye eneo la Kampi ya Moto Ijumaa, waziri huyo alisema kwamba hiyo itakuwa njia moja ya kuimarisha elimu na pia kufanikisha mradi wa serikali ya Jubilee wa kuwapa wanafunzi wa darasa la kwanza vipakatalishi.

“Sio shule zote zimewekwa stima na ninakubali. Kunakaribia shule 3,178, lakini 300 kati yake zimekuwa zikikarabatiwa, na hizo zingine kazi ya kuwekwa stima inaendelea na tunashirikiana na KPLC na REA. Tuliwapa muda wa mwezi mmoja kukamilisha kazi hiyo, wakashindwa na wakaja kuomba muda huo uongezwe. Sitataja hilo tena, na kama wahusika hawataki kufanya kazi, kuna vijana barubaru ambao hawana kazi.”

Aliongeza kuwa, vijana na akina mama wanapaswa kujikakamua ili kuchua kandarasi kutoka kwa serikali za kaunti na ya kitaifa kwa minajili ya kujiendeleza.

Kuhusiana na suala la wizi wa mitambo ya transfoma, waziri Keter alisema: “Wananchi wanapaswa kuwa kwenye mstari wa mbele kufahamisha idara ya usalama kuhusu wezi wa mitambo ya umeme,” pindi tu wanapo waona.

Keter alikuwa ameandama na mwenyekiti wa bodi ya KP Kenneth Marende, katika kufungua kituo kipya kidogo cha kampuni hiyo ya umeme eneo la Rongai.