Kundi moja la akina mama wasomi na wafanyibiashara kaunti ya Kisumu, limezindua kampeni ya kitaifa ya wanawake, kuongoza katika juhudi za kutafuta vitambulisho, kwa kuzingatia umuhimu wa stakabadhi hiyo kwa shughuli mbali mbali za kitaifa.
Akina mama hao kutoka kwenye sekta tofauti tofauti za kijamii wamezindua mpango huo wa kuwahamasisha wenyeji na kuhakikisha wahusika tofauti kwenye jamii wanapokea vitambulisho vya kitaifa, kwa kuzingatia umuhimu wa stakabadhi hiyo.
Mwanasiasa Rosa Buyu ambaye aliwaigombea nafasi ya uwakilishi bunge Kisumu Magharibi katika uchaguzi mkuu uliopita ndiye mshirikishi wa kampeini hiyo.
''Sisi kama wanawake tumeamua kuchukua jukumu la kushinikiza umuhimu wa kuchukuliwa vitambulisho vya kitaifa miongoni mwa vijana, akina mama, wazee na kila mmoja katika jamii,'' alisema Buyu.
Buyu amesisitiza kuwa kando na kaunti ya Kisumu kampeni hii inalenga kaunti zote 47 nchini.