Idara ya usalama eneo la Pwani imelionya kundi la kigaidi la Al Shabaab dhidi ya kupanga njama ya kutekeleza mashambulizi ya kigaidi katika eneo la Pwani kuwa litakabiliwa.
Kamanda mkuu wa polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi, alisema kuwa idara ya usalama inawasaka washukiwa wanne wa ugaidi waliyofanikiwa kukwepa mtego wa maafisa wa kupambana na ugaidi baada ya kuvamia maficho yao eneo la Majengo mjini Mombasa.
Kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Bw Wanjohi alisema tayari kitengo maalum cha maafisa wa usalama kimo nyanjani kuwasaka washukiwa hao ili kuzuia kutokea kwa mashambulizi.
Maafisa wa wa usalama wako macho na wanasaka washukiwa wanne wa ugaidi ambayo wako na uhusiano wa karibu na Al Shabaab ambao wamefanikiwa kukwepa mtego wa maafisa wetu walipovamia maficho yao eneo la Majengo mjini Mombasa," alisema Wanjohi.
Alisema kuwa idara hiyo imepata habari muhimu kuwa washukiwa hao wanne wanauhusiana wa karibu na kundi hilo kwani ni kati ya washukiwa wa ugaidi waliyofanikiwa kutoroka baada ya kujeruhiwa na maafisa wa polisi katika eneo la Kiunga Kaunti ya Lamu.
Tayari maafisa wa usalama, aliongeza Wanjohi, wanashika doria kikamilifu katika kila eneo hapa Pwani ili kuhakikisha kuwa usalama unaimarishwa hata zaidi.