Kundi la kihuni linalijiita 'Wakali Kwanza' linalowahangaisha wakaazi wa eneo bunge la Kisauni limeonywa dhidi ya kutekeleza uvamizi na kutatiza usalama wa wananchi wa sehemu hiyo.
Akitoa onyo hilo siku ya Jumatatu, kamishna ya Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alisema kuwa msako maalumu umeanzishwa kupambana na vijana hao na watakaopatikana watachukuliwa hatua za kisheria.
Marwa aliwataka vijana hao kutojihusisha na visa haramu ili usalama uimarike, na zaidi kuwaonya wanasiasa ambao wanaowatoa vijana hao pindi wanapokamatwa na polisi.
Vilevile, amewataka wazazi wa vijana hao kuwaonya watoto wao dhidi ya kujihusisha na makundi haramu.
Marwa alikuwa akiwahutubia wanahabari ofisini mwake, ambapo aliongeza kuwa licha ya vijana hao kuwa chini ya umri wa miaka 15, watachukuliwa hatua za kisheria kwani ni hatari kwa usalama.
Vijana hao wanahusihwa na visa mbali mbali vya uporaji kwa kutumia silaha kali na hatari.