Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya usalama eneo la Pwani imesema kuwa itaendeleza operesheni ya kuwasaka wafuasi wa kundi lililoharamiswa la Mombasa Republican Council - MRC.

Hii ni kufuatia kutiwa mbaroni kwa wanachama kadha wa kundi hilo la MRC, akiwemo Mwenyekiti Omar Mwamnwadzi.

Akiongea na mwanahabari baada ya kukamilika kwa mkutano wa maafisa wa polisi wa kiusalama siku ya Ijumaa mjini Mombasa, Kamanda wa Polisi wa Utawala Kaunti ya Kwale James Akoru, alisema kuwa atafanya kila juhudi ili kuhakikisha kuwa kundi hilo linaangamizwa.

Akoru alieleza kuwa kundi hili linatishia kuzorotesha uchumi wa eneo la Pwani, kwani wawekezaji wengi kutoka nje ya eneo hili huogopa kuwekeza hapa Pwani.

“Kama idara ya usalama tutahakikisha kuwa hakuna kundi lolote la kihalifu linatatiza usalama wa eneo hili na tutahakikisha kuwa makundi kama hayo yanaangamizwa na kuimarisha usalama wa eneo zima la Pwani,” alisema Akoru.

Wakati uo huo Akoru amewataka vijana wa eneo hili wajiepushe na harakati za makundi yalioharamiswa.

Akoru aliwahimiza vijana wajiunge na vyuo vya kiufundi na taasisi nyingine za masomo ili wajiendeleze kiamendeleo, huku akiitaka jamii isikubali kadi za uwanachama za kundi hilo zinazouzwa.