Share news tips with us here at Hivisasa

Kundi la Mombasa Republican Council, MRC, ambalo lasemekana limeanza kuchukua mkondo mpya baada ya baadhi ya wazee kusambaza vikadi vya usajili mpya wa kundi hilo limeonywa vikali dhidi ya visa hivyo.

Akihutubia wananchi wakati wa maadhimisho ya sherehe za Jamhuri katika uwanja wa Tononoka mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mshirikishi mkuu wa serikali eneo la pwani Samuel Kilele amelitaka kundi hilo kusitisha harakati hizo.

Kilele amewatahadharisha wakazi dhidi ya kugawanywa na kundi hilo, huku akisema kwamba tayari maafisa wa polisi wanawasaka wafuasi hao ili kuwakabili.

“Tunayaonya makundi ya kihalifu kusitisha mara moja harakati zao na kudumisha amani kabla ya kuandamwa na maafisa wa polisi kwani serikali kamwe hataruhusu makundi yatekeleza uhalifu, tunataka kila mtu kudumisha amani,” alisema Kilele.

Wakati huo huo, Kilele amewasisitizia wakazi wa Kaunti ya Mombasa kushirikiana na maafisa wa usalama katika kuwafichua wahalifu wanaolenga kuzuru usalama wa eneo la Pwani ili amani kudumishwa.

Amesema kwamba serikali ya kaunti itahakikisha kuwa ugatuzi unaendelezwa, huku akitoa hakikisho la kuendeleza ushirikiano na serikali za kaunti ili kuona kwamba wananchi wanatekelezewa maendeleo.