Share news tips with us here at Hivisasa

Kundi la Mombasa Republican Council (MRC) limeonywa dhidi ya kusambaza vikaratisi na kuwasajili vijana kujiunga na kundi hilo ili kutekelezwa uvamizi katika maeneo mbalimbali Pwani.

Akitoa onyo hilo katika mkao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Kamanda mkuu wa polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi alisema kundi hilo lilikuwa likisajili vijana na kuwapa vitambulizi bandia vya kundi hilo katika eneo la Diani, Ukundi, Kaloleni na kisiwani Mombasa.

Wanjohi alisema kwamba tayari maafisa wa polisi wametumwa kuwasaka wanaotekeleza njama hiyo ili kuwatia nguvuni na kusitisha hofu iliyotanda katika maeneo ya wakazi huku akiwataka wakazi kutoa habari muhimu kuhusu kundi hilo.

"Tunalionya kundi hilo la MRC kusitisha harakati zake za kuwasajili vijana na kuwapa vitambulisho bandia vya kundi hilo la sivyo maafisa wa polisi wataliandama mora moja kwani serikali haiwezi ruhusu vikundi vinahangaisha wakaazi,"alisema Wanjohi.

Kwa upande wake Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alisema kwamba lazima kundi hilo kusitisha harakati zao kabla ya maafisa wa polisi kuwaandama na kuwakabili kisheria huku akiwataka wazazi wa vijana hao kuchukua jukumu la kuwaonya vijana wao.

"Tunawahimiza wazazi wa vijana hao kuwaonya vijana wao na mapema na kujitenga na kundi hilo la MRC kwa sababu serikali haiwezi ruhusu watu wachache kuangaisha usalama wa wakenya wanaopenda amani," alisema Marwa.  

Kauli ya viongozi hao wa usalama hapa pwani imejiri baada ya kuchipuka madai kuwa baadhi ya viongozi wa kundi hilo katika eneo la kusini mwa pwani wameanza usajili wa vijana na kuwapa vikadi kama vitambulisho vya kuchipuka upya kwa kundi hilo.