Wakazi wa eneo la Mgombezi wametoa maoni tofauti tofauti kufuatia hatua ya mrengo wa Cord kuliondoa jina la mbunge wa eneo hilo, Khatib Mwashetani kwenye kamati inayowaleta pamoja wanachama 29 wa kutoka mirengo ya upinzani na ile ya serikali.
Salim Mwaviriko ambaye ni mkazi wa eneo hilo amesema kuwa hilo walikuwa wamelikisia kuwa litatokea kufuatia hatua ya mbunge huyo kujitokeza hivi majuzi na kuonekana kukumbatia sera za chama kipya cha serikali cha JAP.
"Huwezi kuasi chama kilichokupeleka wewe bungeni na ukadhani kuwa hutochukuliwa hatua yoyote. Kwa hiyo mimi naona mheshimiwa amepata haki yake sasa yuko huru kujiunga na chama hicho," aliendelea Salim.
Mkazi mwinigine Mzee Zecha, akiongea na mwandishi huyu ameunga mkono matamshi ya Salim, na kusema kuwa hawajapata manufaa yoyote tangu walipomteua mbunge huyo kuwawakilisha na hivyo wao wanaipongeza Cord kwa hatua hiyo ya kumuondoa.
"Sasa tutaangalia kiongozi mwingine mwenye ari ya kuhudumia wananchi. Hapa mgombezi hatuna chochote cha kujivunia kutoka kwa serikali ya kaunti wala kuu na sasa wakati umewadia wa mbivu na mbichi kujulikana," alitoa kauli yake.
Hata hivyo, mkazi mwingine Salma Mwadziya alisema kuwa uongozi wa mrengo ungempa nafasi nyingine ya kujituma mbunge huyo kwani pengine angebadili mawazo ya kukihama chama.
Wabunge wengine ambao huenda wakachukuliwa hatua na Cord ni pamoja na mbunge wa Ganze Peter Shehe, Salim Mustafa wa Kilifi Kusini, James Kamoti wa Rabai na Gideon Mung'aro wa Kilifi kaskazini.