Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Gatundu kusini, Moses Kuria amesema kuwa atataja majina ya viongozi wa CORD waliohusika na sakata ya NYS.

Kuria alisema kuwa Waiguru ana muda wa kutosha kuyataja majina ya wabunge 52 wa mirengo ya Jubilee na CORD waliohusika na sakata hio.

‘‘Katika wiki mbili zijazo, viongozi wa Jubilee watatilia maanani usajili wa wapiga kura. Waiguru achukue fursa hiyo na awataje wote wanaohusika na sakata ya NYS,’’ alisema Kuria.

Akizungumza kwenye harambee katika kanisa la Hope of Family lililoko Githurai, Kuria pia alimkashifu Waiguru kwa ubaguzi katika kutaja majina ya waliohusika na sakata ya NYS.

Mbunge wa Ruiru, Esther Gathogo ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema kuwa kuhusishwa kwa viongozi wa mrengo tawala wa Jubilee na sakata za ufisadi ni njama ya mrengo wa upinzani kuwashawishi wafuasi wa Jubilee kutojisajili kama wapiga kura.

Bi Gathogo aidha aliwaagiza wakaazi wa Nairobi kutomchagua Bi Waiguru kama gavana wa kaunti ya Nairobi kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa usemi kuwa alishindwa kuongoza shirika la NYS.

‘‘Hakuna haja ya kumchagua mtu ambaye alishindwa kumaliza muhula wake kufuatia madai ya ufisadi kwani hata akichaguliwa kama gavana hatamaliza muhula wake,’’ alisema Bi Gathogo.