Mshauri wa Benki ya Dunia tawi la Kenya Charles Mochama ameshtumu hatua ya baadhi ya wakazi wa Kaunti ya Nyamira kuingisha unyumba katika chaguzi mbalimbali za kisiasa.
Akihutubia wakazi wa Mochenwa Mochama alisema kuwa baadhi ya wakazi wa kaunti hiyo wanaendelea kushikilia unyumba, hali aliyosema itaathiri pakubwa ukuaji wa Kaunti ya Nyamira, huku akiwahimiza wakazi kuwasuta viongozi wanaopigia upato chaguzi za unyumba na kuzigatia kuwachagua viongozi kulingana na utendakazi wao.
"Nashangazwa sana na baadhi ya viongozi wanaoshinikiza viongozi wa kisiasa kuchaguliwa kutokana na misingi ya unyumba, na hilo ni wazo ambalo linafaa kutupiliwa mbali, na ni himizo langu kwa wakazi wa kaunti hii kuhakikisha kuwa wana wachagua viongozi kulingana na rekodi ya utendakazi wao kwa maana siasa za unyumba zitasababishia watu wetu umaskini kutokana na uongozi mbaya," alisema Mochama.
Mochama aliongeza kusema kuwa baadhi ya viongozi wengi nchini wametumia unyumba kuwagawa wakenya kwa misingi ya kikabila, hali inayofanya iwe vigumu kwa serikali za kaunti kukabiliana na visa vya ufisadi, akihoji kuwa iwapo hali hiyo itaendelea kushuhudiwa nchini, wananchi wataendelea kuteseka pakubwa.
"Hili suala la kuwachagua viongozi eti kwa sababu wanatoka kwenye jamii yako linaathiri pakubwa ukuaji wa taifa, na hata huwa vigumu kwa mashirika ya kupambana na ufisadi kuwakabili viongozi husika kwa maana kuwa viongozi husika husitiriwa na wanajamii wao," aliongezea Mochama.