Mamlaka ya maendeleo ya KVDA imezindua mpango wa kuboresha mazingira kupitia kwa miradi ya maendeleo ambayo huendelezwa na shirika hilo.
Shirika hilo limesema mpango huo unalenga kuboresha mazingira katika maeneo lengwa mbali na kuimarisha uzalishaji wa chakula na kukabiliana na umaskini katika maeneo kame.
Mwenyekiti wa shirika hilo Sammy Kona alisema shirika hilo limejitolea mhanga kuafikia sera ya serikali ya kupanda miti kwa aslimia 10 katika ardhi yote kote nchini.
Akihutubia wana habari katika makao makuu ya shirika hilo mjini Eldoret Kona alisema KVDA ina mipango ya kushirikiana na jamii kupanda miti zaidi katika vyanzo vya maji katika maeneo ya Cherang’any na misitu mingine katika eneo la Kaskazini mwa Rift Valley Kenya.
Ili kuafikia malengo hayo shirika hilo linalenga kuimarisha mapato yake na kufikia bilioni 200.
“Kama KVDA tunapanga kushirikiana na wadau wengine kuboresha mapato yetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ambapo tunalenga kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha huduma zetu,” alisema Kona.
Naye mkurugenzi wa shirika hilo David Kimosop alisema shirika hilo linataka kuhusisha wananchi katika maeneo ambako shirika hilo huhudumu katika maswala ya utunzi wa mazingira.
Kimosop alisema mpango huo umehusihwa katika mikakati ya miaka mitano ya kuboresha huduma zake.
“Katika miaka hii mitano tunataka kuhusisha wadau wote ikiwa ni pamoja na wanafunzi katika upanzi wa miti na maswala ya utunzi wa mazingira kwa jumla,” alisema.
Mradi wa utunzi wa mazingira utazinduliwa katika eneo la Ravine kaunti ya Baringo ambapo shirika hilo litazindua mradi wa upanzi wa miti katika ekari 45 shughuli ambayo itaongozwa na waziri wa mazingira Judy Wakhungu.
Mbali na utunzi wa mazingira shirika la KVDA linalenga kupanua uzalishaji wa maendeo North-Rift. Kwa mujibu wa Kimosop ni kwamba shirika hilo linapania kupanda miti milioni 5 ya maembe.
Tayari kaunti ya Baringo imepanda milioni 1.7 ya miti ya maembe kama awamu ya kwanza ya mradi huo. Ili kuafikia malengo yake shirika hilo linapania kukusanya shilingi milioni 300 kwa mapato yake kila mwaka.